Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa mujibu wa WHO, kirusi kipya cha corona cha India kimeshaenea pia katika nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Kenya, Afrika Kusini na Uganda.
Taarifa ya kuenea corona huyo wa India katika nchi 49 duniani imetolewa katika hali ambayo India imevunja rekodi nyingine ya vifo vya corona kwa siku moja. Kwa mujibu wa taarifa, watu 4,205 wamepoteza maisha kwa COVID-19 katika kipindi cha siku moja nchini India, ikiwa ni rekodi mpya ya idadi kubwa ya watu wanaokufa kwa ugonjwa huo kwa siku, duniani. Hadi hivi sasa watu 250,000 wameshapoteza maisha kwa corona nchini India pekee huku idadi ya maambukizi nayo ikiongezeka na kupindukia watu milioni 23 baada yakesi nyingine 349,421 za maambukizo ya corona kuripotiwa kwa siku moja katika nchi hiyo ya Asia.
Jumatatu wiki hii, WHO ilitangaza kuwa, kirusi cha kipya cha corona kilichogunduliwa India kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba mwaka jana ni hatari kwa dunia nzima hasa kwa vile maambukizi yake ni ya haraka na mepesi sana.
Athari za ugonjwa wa corona nchini India ni kubwa mno kiasi kwamba, baadhi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo siku chache zilizopita viliripoti kuwa, kuwa viwiliwili vya watu waliofariki kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo vimeonekana vikielea kwenye Mto mkubwa wa Ganga wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The Times of India, maiti kadhaa wa wagonjwa wa corona wameonekana wakielea kwenye fukwe za mto huo katika maeneo ya mji wa Buxar ulioko kwenye mpaka wa majimbo mawili masikini ya India ya Bihar na Uttar Pradesh.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, tukio hilo la karibuni linadhihirisha ukubwa wa kiwango cha usambaaji wa kirusi cha corona na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 hadi kwenye maeneo ya mbali ya India.
342/